international news


Maandamano yasitishwa Cuba

Kundi maarufu linaloipinga serikali ya Cuba limesitisha maandamano yake ya kila wiki kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kumi na tatu kufuatia kifo cha Fidel Castro ambaye wao wamekuwa wakimpinga kwa miaka yote.

Kiongozi wa kundi hilo la wanawake maarufu kama Ladies in White, Berta Soler, amesema ametaka kutoa fursa kwa wengine kuomboleza na hivyo hatasheherekea kifo cha mtu yeyote.

Maandamano hayo ya wanawake ya kila wiki ni kwa lengo la kuwaunga mkono waume zao waliofungwa kwa sababu ya kuipinga serikali. Kumekuwa na hali ya simanzi katika mji mkuu wa Havana siku kilipotangazwa kifo cha Fidel Castro. Mwandishi wa BBC mjini humo amesema watu bado wapo katika mshtuko.

Baadhi ya raia mjini Havana wanasema wameanza kukubaliana na hali halisi:

Lazaro Alonso, anasema " Ni vigumu sana kukubali, lakini ndivyo maisha yalivyo. Tunaendelea kufanya kazi kwa bidii, kusonga mbele, hakuna kitakachozuia huo mchakato, na tunatahadhari kwamba ndio, iko siku mambo makubwa yatatokea nchini humu."

Victor Manuel, naye amenukuliwa akisema "kwetu sisi, kamanda wetu ndio baba wa familia, baba wa mapinduzi, baba tuliyekuwa nae, ambae siku zote na leo tunahisi tumempoteza katika maisha yetu."

Leo Jumatatu, Cuba inaanza siku tisa za maombolezo rasmi.

Taarifa na Yohana Dioniz kwa msaada wa Tovuti ya BBC Swahili.


Fillon amshinda Juppe kwenye mchujo Ufaransa

Francois Fillon ndiye atakayekuwa mgombea urais wa chama cha wahafidhina nchini Ufaransa baada ya mpinzani wake Alain Juppe kukubali kushindwa.

Baada ya kura nyingi kuhesabiwa, bw Fillon alikuwa anaongoza akiwa na karibu asilimia 67 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi wa mchujo Jumapili.

Bw Fillon ameahidi kuunda jamii yenye usawa na haki zaidi, akisema Ufaransa inahitaji "ukweli an inahitaji hatua zichukuliwe".

Sasa huenda akakabiliana na mgombea wa chama cha Kisosholisti na mgombea wa chama cha mrengo wa kulia Marine Le Pen uchaguzini mwezi Aprili.

Bw Juppe, ambaye siasa zake sana ziliegemea msimamo wa wastani, alimpongeza Bw Fillon kwa ushindi wake "mkubwa" na akaahidi kumuunga mkono katika juhudi zake za kutana kuwa rais.

Baada ya kura kutoka vituo 9,713 kati ya 10,229 kuhesabiwa, Fillon alikuwa ameshinda 66.6% naye Bw Juppe 33.4%.

Taarifa na Yohana Dioniz kwa msaada wa Tovuti ya BBC Swahili.


Edgar Lungu na Idriss Deby wako Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu aliwasili nchini Tanzania kwa ziara ya kiserikali ya siku 3 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.

John Pombe Magufuli.Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Lungu amepokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli na kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali nchini humo pamoja na wananchi.

Akiwa uwanjani hapo Rais Lungu amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Rais Lungu ataendelea na ziara yake ambapo pamoja na kutembelea miradi ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo TAZARA na TAZAMA, atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli, atashuhudia utiaji saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia na jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Magufuli kwa ajili yake Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Chad Mhe. Idriss Deby Itno naye amewasili nchini Tanzania kwa ziara kikazi ya siku 2.Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Rais Idriss Deby Itno akiwa na Mkewe Mama Hinda Deby amepokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na wananchi. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Rais Idriss Deby Itno Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Taarifa na Yohana Dioniz kwa msaada wa Tovuti ya BBC Swahili.

our programs

Sikiliza kila siku ya wiki kuanzia saa 06:00am hadi 06:30am
Sikiliza kila siku ya wiki kuanzia saa 06:30am hadi 07:00am
Sikiliza kila siku ya wiki kuanzia saa 07:30am hadi 08:00am
Sikiliza kuanzia 2:00pm - 4:00pm jtatu hadi Alhamisi
kuanzia saa 2:00pm - 4:00pm FRIDAY only